UHIFADHI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Ili kitu kidumu ni lazima kihifadhiwe; fasihi simulizi kama sanaa kutokana na umuhimu wake katika jamii nayo huhufadhiwa kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho. Katika mada hii utaweza kujifunza umuhimu wa fasihi simulizi katika jamii. Utajifunza njia mbalimbali zitumikazo katika uhifadhi wa fasihi simulizi pia utaweza kubainisha ubora na udhaifu wa kila njia.
Kuhifadhi Fasihi Simulizi
Bainisha njia za kuhifadhi fasihi simulizi
Umuhimu wa kazi za fasihi simulizi
Ingawa kila utanzu wa fasihi una umuhimu wake, kwa pamoja tanzu zake zote zina umuhimu mkubwa katika jamii.
Kwaza fasihi hutumika kama chombo cha kuwaelimisha watu. Kupitia fasihi andishi na fasihi simulizi, watu hupata maarifa ya kutambua mambo maovu na namna ya kuyakwepa. Licha ya haya, wanajamii hujifunza njia za kujitawala, kuzalisha mali na kuishi kwa misingi ya haki, usawa na demokrasia.
Pili, fasihi ni nyenzo ya kutoa mafunzo kuhusu mambo kama vile historia, dini, siasa, jiografia na tiba. Kwa hiyo watu hujifahamisha juu ya maumbile na asili yake, mazingira, utawala, uchumi, sheria n.k.
Aidha fasihi huwapa watu mazoezi na kuimarisha uwezo wao wa kuzungumza kwa ufasaha, kuimba nyimbo kwa ufundi, kuigiza mambo kwa ustadi, kucheza ngoma kwa umahiri, kughani mashairi kwa mvuto na kusimulia matukio kwa mtindo ufaao.
Fasihi hufahamisha, huhifadhi na hurithisha mambo kuhusu utamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mambo hayo ni pamoja na mila, desturi, falsafa, imani na itikadi. Pia hudumisha maarifa ya kijadi kama vile tiba, sayansi ya kilimo, uhifadhi wa mazingira na sayansi ya utabiri wa hali ya hewa.
Umuhimu mwingine wa fasihi unatokana na kutumika kwake kama chombo cha kuburudisha na kupumbaza. Watu wanaposoma kazi mbalimbali za fasihi hupata, msisimko wa kimwili na kiakili. Kadhalika fasihi hugusa hisia za watu na kuwafanya wafurahi au wahuzunike.
Istoshe fasihi hudumisha na kukuza lugha. Watu hupanua msamiati wao na miundo ya lugha kupitia kazi zake. Hivyo fasihi inakuwa kama hazina ya maneno na dafina ya kanuni za kisarufi.
Kutokana na umuhimu huu ndio maana fasihi huhifadhiwa ili isipotee. Na uhifadhi huu hufanyika kwa njia mabalimbali.
Ubora na Udhaifu wa kila Njia ya Kuhifadhi kazi za Fasihi Simulizi
Elezea ubora na udhaifu wa kila njia ya kuhifadhi kazi za fasihi simulizi
Fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa kwa njia zifuatazo:
Kichwani
Hii ndio njia ambayo imekuwa ikitumiwa kuhifadhi kazi za fasihi tangu kale na inaendelea kutumika hadi leo. Kwa kutumia njia hii kazi ya msanii hukaa kwenye ubongo wa msanii, naye huweza kuiwasilisha kazi hiyo, wakati wowote bila gharama yoyote.
Ubora wake
  • Uwasilishaji wa kazi hiyo unaweza kufanyika wakati wowote bila kuhitaji kufanyika maandalizi yoyote, hususani ya kiufundi.
  • Hakuna gharama yoyote wakati wa uwasilishaji wa kazi ya fashi. Msanii hahitaji kugharimia kitu chochote ili waweze kuitoa kichwani, ni uamzi wake tu, anaweza kuimba papo kwa papo.
  • Kazi ya fasihi iliyohifadhiwa kichwani ni hai. Hii ni kwa sababu msanii anakuwa ana kwa ana na hadhira yake. Kutokana na matumizi ya mbinu tofauti za kisanaa kama vile kucheza, kubadili sauti, miondoko na mengineyo mengi, kazi yake inapata uhalisia zaidi mbele ya hadhira.
Udhaifu wake
  • Uwezekano wa kazi kupotea au kuharibika hasa katika fani ni mkubwa. Kwa mfano msanii anapokuwa amefariki dunia kazi anayokuwa ameihifadhi kichwani nayo hupotea. Ndio maana katika baadhi ya jamii kazi za kifasihi zimepotea. Hii ni kwa sababu wasanii wanapoondoka duniani hondoka na fani hizo.
  • Kazi inapohifadhiwa kichwani ni rahisi kubadilika. Hii inatokea pale ambapo msanii anasahau baadhi ya maneno kutokana na umri wake au sababu nyinginezo
Njia ya maandishi
Maandishi ni njia moja wapo inayotumika kuhifadhia kazi za fasihi. Njia hii imeanza kutumika baada ya watu kujua kusoma na kuandika. Uhifadhi wa kazi za fasihi kwa njia hii hupitia njia mbili kubwa. Hatua ya kwanza ni kubuni kisa au wazo; na hatua ya pili ni kuliweka wazo hilo katika maandishi. Kazi za fasihi simulizi zinazoweza kuhifadhiwa katika maandishi ni hadithi, nyimbo, mashairi, ngonjera, majigambo n.k
Ubora wake
  • Kazi iliyohifadhiwa inaweza kudumu kwa muda mrefu
  • Kazi iliyohifadhiwa inaweza kufikia hadhira hata ya mbali na aliko msanii.
  • Kazi iliyohifadhiwa katika maandshi haipotezi fani yake na maudhui yake bali huendelea kuwa katika asili yake ya awali hadi msanii atakapoamua kuibadilisha.
Udhaifu wake
  • Hii njia ni kwa ajili ya watu wachache tu wanaojua kusoma na kuandika.
  • Wasanii wanaoweza kutumia njia hii ni wale tu wanaojua kusoma na kuandika.
  • Ni aghali sana kuhifadhi kazi za kifasihi kwa njia ya maandishi. Msanii atalazimika kununua vifaa vinavyohitajika katika maandishi ambavyo ni kalamu, karatasi, meza. Kwa hiyo ni aghali.
  • Uwasilishaji wake si hai kwani hakuna kuonana ana kwa ana kati ya hadhira na fanani. Kwa hiyo msomaji hawezi pata vionjo vya msanii hivyo itambidi ajibunie yeye mwenyewe.
  • Wahusika pia hawawezi kuonekana, endapo ni igizo mabalo limehifadhiwa katika maandishi, hivyo ubora wa kazi ya msanii huchujuka.
Njia ya vinasasauti
Vinasasauti ni miongoni mwa vyombo vinavyotumika kuhifadhi kazi za fasihi simulizi. Hii ni njia iliyoendelea kuliko ile ya maandishi.
Ubora wake
  • Kazi ya msanii huweza kuwafikia watu hata walio mbali na alipo mtunzi.
  • Ikihifadhiwa katika vinasasauti kama vile tepurekoda au CD ubora wake huwa haupotei wala kuharibika endapo vifaa hivyo vitatunzwa vizuri.
  • Sauti ya mtunzi unaiskia moja kwa moja
  • Unaweza kusikia vionjo vya msanii
Udhaifu wake
  • Njia hii ni aghali kutumia, kununua vinasasauti ni gharama.
  • Uwasilishaji wake si hai, ingawa unaweza sikia sauti ya msanii au wahusika lakini hahawezi kuonekana.
  • Kazi yoyote ya kifasihi inapohifadhiwa katika vinasasauti, kwa mfano nyimbo, huwa ni mali ya msanii husika, mtu yeyote haruhusiwi kuitumia kama mali yake binafsi bila kuruhusiwa na msanii.
Njia ya kompyuta
Njia hii imeanza kutumika katika miaka ya hivi karibuni baada ya watu kuanza kujua na mna ya kutumia kompyuta.
Ubora wake
  • Njia hii ni ya uhakika zaidi kwa vile shuguli za kisanaa zinazohusika huhifadhiwa katika kompyuta na hutolewa pale zinapokuwa zinahitajika.
Udhaifu
  • Msanii au wasanii wanohusika hawawasiliani na hadhira papo kwa papo. Hivyo hadhira hukosa kuuliza maswali katika vipengele vinavyotatiza.
  • Ili kuhifadhi kazi ya fasihi kwa kutumia njia hii ni sharti msanii awe anajua kutumia kompyuta.
  • Pia ni aghali sana, kuzingatia kwamba kununua komputa ni gharama kubwa.
Njia ya kanda za video
Msanii huweza kutumia kanda ya video kuhifadhi kazi yake.
Ubora wake
  • Kwanza wasnii na vifaa wanavyotumia huonekana
  • Sauti zao na milio ya ala wanazotumia husikika na pia huonekana kwa hadhira. Hii angalau huipa uhai kazi ya msanii mbele ya hadhira.
  • Huweza kudumu kwa muda mrefu endapo kanda ya video iliyotumika kuhifadhi kazi ya msanii itatunzwa vizuri.
Udhaifu wake
  • Uhifadhi wa njia hii ni aghali, msanii atahitajika kununua, kanda ya video, kumlipa mpiga picha na mzalishaji pia.
  • Watu wanoweza kunufaika na njia hii ni wacheche mno na wengi wao ni wale wenye uwezo wa kumiliki televisheni ambao kimsingi hupatikana maeneo ya mijini.
  • Ingawaje hadhira wanaweza kumwona msanii lakini hawawezi kuwasiliana nae ana kwa ana, hivyo kukosa kuuliza swali pindi wanapohitaji kufanya hivyo.

Faida ya Kuhifadhi Fasihi Simulizi
Elezea faida ya kuhifadhi fasihi simulizi
Njia zote za uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi zina umuhimu mkubwa katika ukuzaji na uendelezaji wa utamaduni katika jamii. Kama ambavyo tumekwishaona, kazi za fasihi simulizi huelimisha, huburudisha, hurithisha maarifa, maadili, pia ni vielelezo vya utamaduni wetu wa asiili. Kwa ajili hiyo ni muhimu kuzihifadhi kazi hizo zisiharibike wala kupotea ili ziendelee kutumika kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Ni muhimu ziendelee kuwepo ili kuhifadhi utamaduni wetu na huku vikitumika kama vivutio vya watalii.
Kazi za fasihi simulizi kwa upande mwingine ni sehemu ya ajira. Kwa mfano, shughuli mabalimbali za kisanaa kama vile ngoma, maigizo na utunzi wa vitabu, vinawapatia vipato baadhi ya wasanii. Hivyo ni muhimu zihifadhiwe.
Kazi za fasihi simulizi pia ni kichocheo cha umoja na maelewano miongoni mwa jamii. Yote hayo kwa ujumla wake yanabainisha kuwepo na haja ya kuendelea kuzikusanya, kuzifanyia kazi, kuziendeleza, na kuzihifadhi kazi za fasihi simulizi.



logoblog

No comments:

Post a Comment